View this article in English | bilingual

Mamba

Nami nambe, niwe kama waambao
Niupambe, upendeze wasomao
Niufumbe, wafumbuwe wawezao
 
Kuna mamba, mtoni metakabari
Ajigamba, na kujiona hodari
Yuwaamba, kwamba ‘taishi dahari
 
Memughuri, ghururi za kipumbavu
Afikiri, hataishiwa na nguvu
Takaburi, hakika ni maangavu
 
Akumbuke, siku yake ikifika
Roho yake, ajuwe itamtoka
Nguvu zake, kikomoche zitafika
 
Afahamu, mtu hajuwi la kesho
Hatadumu, angatumiya vitisho
Maadamu, lenye mwanzo lina mwisho.