Skip to content
We’re hiring a books editor! Learn more and apply by August 6.
from the May 2013 issue

Watumwa wa Uchochole

Baada ya uhuru, shindano jipya lilianza. Shindano la mbio za kujitajirisha. Mbunge mmoja aliyechukizwa na hali hii aliieleza kama “uhuru na kunyang’anyana”. Kaida ya mashindano ya mbio ni kwamba wakimbiaji huanzia kwenye mstari mmoja. Lakini mashindano haya ya mbio za kujitajirisha hayakufuata kaida hii. Mbio zilipoanza, baadhi ya wakimbiaji walikuwa mbele ya wengine. Waliokuwa mbele ni wachache waliofaidika kutokana na utawala wa kikoloni. Walimsaidia mkoloni kuwagandamiza Waafrika wenzao, naye mkloni akawatunza. Hawakukosea waliosema kuwa mcheza kwao hutunzwa. Hawa ndio waliokuwa mstari wa mbele kuhalalisha utabaka. Walisikika mitaani, vijijini na hata katika ofisi za serikali wakisema: “Usawa ni ndoto. Binadamu hawawezi kuwa sawa. Lazima kuwe na wafupi na warefu; wanene na wembamba; matajiri na maskini”

Mwelekeo huu ulisaidia sana kuwashawishi wananchi kukubali kuishi katika umaskini wa kupindukia. Waliyaona kuwa ni majaliwa. Hali kama hii ilipatikana katika Kijiji cha Gituge. Hapa ndipo umaskini ulipojenga zizi lililoendelea kupanuka kila uchao. Kijiji hiki kilikuwa katika sehemu ya nchi ambayo haikuwa na utajiri wa mimea ya kuleta fedha. Tabianchi na udongo wa eneo hili havikuendana na upanzi wa kahawa, pareto, majani chai, miwa wala tumbaku. Wakulima wadogo wa Gituge – ambao walikuwa wachochole – walitegemea mimea ya chakula iliyozaa maharagwe, mahindi, ndizi na viazi.

Haya ndiyo mazingira ambamo Riuki alizaliwa na kulelewa. Jina lake hasa lilikuwa Muriuki lakini lilifupishwa kama ishara ya upendo. Mwishowe, kifupi chake, yaani Riuki, kikazoeleka kiasi kwamba jina kamili lilielekea kuzikwa kaitika kaburi la sahau. Riuki alipendwa na vijana wa rika lake kutokana na usafi wa roho yake, uchangamfu na wingi wa vipawa vyake. Alikuwa mchezaji wa mchezo uliopendwa sana na uliokuwa na mashabiki wengi. Huu ulikuwa mchezo wa kandanda. Lakini ni katika masomo ambapo alijitambulisha kama kijana mwnye kipaji cha kipekee. Alipita mitihani yake kwa alama za juu sana. Mwalimu wake wa hisabati – Padre M’Arache, alimpa zawadi ya saa.

Siku hizo, kilele cha ufanisi katika masomo kilikuwa kuteuliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere. Hiki ndicho kilele ambacho Riuki alikuwa amekilenga (zutafindaki hii ilisimama juu ya kilima kimojawapo mjini Kampala) na hatimaye kukifikia. Baada ya kufika kileleni Makerere, Riuki alikuwa shujaa wa kijiji cha Gituge. Alikuwa wa kwanza kupata ufanisi kama huu masomoni.

Babake Riuki alikuwa makanika. Alipata riziki yake kwa kukarabati magari katika mji wa Ugene ambao ulikuwa makao makuu ya wilaya. Mji huu ulikuwa umbali wa kilomita tatu hivi kutoka kijiji cha Gituge. Vijana wengi kutoka kijijini waliacha masomo na kwenda mjini kufanya kazi uchwara kama vile kuhudumu katika mikahawa na vilabu. Riuki alishakataa kufuata njia hii iliyopelekea kwenye shimo la umaskini. Babake alikuwa mlevi wa kupindukia. Mapato yake yote yaliishia kwenye pombe. Kweli cha mlevi huliwa na mgema. Magaju hakuwajibika kama mzazi. Hata karo ya Riuki alikuwa ameshindwa kuilipia. Kakake, baba mkubwa wa Riuki, pamoja na mkewe ndio waliochukua mzigo wa kulipia masomo yake. Mwiraria na mkewe walimtunza Riuki kama mtoto wao waliyemzaa. Riuki alimchukulia mke wa babake mkubwa kama mamake wa pili. Walipendana sana.

Ndoto mojawapo ya Riuki ilikuwa kuutumia mshahara wake wa kwanza kuwaonyeshea shukrani mama zake wawili. Alidhamiria kuwanunulia zawadi iliyotoshana na fadhili nyingi na mapenzi yasiyoelezeka kutoka kwao. Hali hii iliifanya kazi ya masomo kuwa kama mchezo kwake.

Hauchi hauchi unakucha. Riuki alimaliza masomo yake akapata shahada ya BSc. Katika somo la hisabati. Siku hizo hakukuwa na shida ya ukosefu wa ajira kwa watu wenye shahada. Kwa hivyo Riuki alipata kazi pindi tu alipomaliza masomo yake. Aliajiriwa na serikali kama ofisa wa uhasibu katika makao makuu ya wilaya.

Riuki aliamini katika usemi kwamba ahadi ni deni. Alikuwa ameahidi kuwaonyesha shukrani mama zake kwa juhudi zao za kumsaidia na kumtia moyo masomoni. Japokuwa hakuitamka ahadi hii kwa mtu yeyote, aliona sasa kwamba wakati wa kuitimiza ulikuwa umewadia. Kwa muda, aliwazia zawadi ambayo ingefaa kwa mama zake. Hatimaye alifikia uamuzi. Alipoupokea mshahara, aliketi na kupanga bajeti. Kisha akaenda madukani na kununua blanketi mbili nzito, sufuria nne kubwa za kupikia, leso nne na sahani za kaure darzeni mbili. Mpango wake ulikuwa kwamba mama zake wangegawana zawadi hizi nusu kwa nusu. Alikodisha gari la kubeba bidhaa hizi kutoka mjini hadi nyumbani.

Mamake mzazi ndiye aliyemkuta nyumbani. Alipoulizia juu ya mamake wa pili, alijibiwa kwamba alikuwa ametoka kwenda kutafuta kuni.

“Basi mama, mimi narudi zangu kazini. Mwenzako akirudi mpelekee zawadi zake. Mpe blanketi moja, leso mbili, sufuria mbili na sahani darzeni moja”, alisema huku akiingia kwenye teksi iliyomleta.

“Sawa mwanangu. Mungu akubariki”, mamake alijibu.

Gari liling’oa nanga na kuondoka.

Riuki alimwamini mamake, kwa hivyo hakuona haja ya kufuatilia kuhakikisha kwamba mamake wa pili alipata zawadi zake. Aliendelea na shughuli zake za kazini. Alitoka nyumbani kila siku asubuhi na kutembea hadi ofisini kwake mjini. Aliipenda kazi yake, kwa hivyo aliifanya kwa bidii na kwa furaha.

Siku mbili zilipita. Siku ya tatu akirudi nyumbani kutoka kazini alikutana na mamake wa pili akitoka mtoni kuchota maji. Riuki alimhurumia. Maskini Bibi Mwiraria hakuwa na mtoto. Alikuwa tasa – dosari kubwa kabisa kijijini. Ilibidi afanye kazi zake za nyumbani zote mwenyewe. Wanawake wa rika lake walikuwa na watoto wa kutuma kuchota maji, kuokota kuni, kuchuma mboga na kwenda kununua kiberiti madukani.

“Mama hujambo!” Riuki alimsalimia kwa bashasha.

“Sijambo mwanangu. Habari za kazi?”

“Nzuri. Nzuri tu mama. Naipenda kazi yangu”, Riuki alijibu.

“Vizuri. Nafurahi kusikia hivyo”.

“Unajua nini mama?”

“Niambie mwanangu”.

“Katika miaka michache ijayo dhiki hii ya kubeba mtungi mgongoni kutoka mtoni itatuondokea. Nitafanya juu chini kuhakikisha kwamba watu wa kijiji chetu wanaletewa maji ya mabomba”.

“Tuna bahati kuwa na mtoto ambaye yuko karibu na serikali. Waeleze taabu zetu. Mara nyingine nahisi kama kwamba kijiji chetu kilisahauliwa. Ni kama tuliachwa tuangamie katika umaskini. Yako wapi matunda ya uhuru tulioahidiwa?”

“Labda matunda ya uhuru yana wenyewe. Hata hivyo tusife moyo mama. Nina matumaini kwamba tutapata usaidizi hivi karibuni. Umaskini sio hali ya kudumu wala majaliwa. Unaweza kuondolewa. Dawa yake ni maendeleo. Tukianzisha miradi kama vile kusambaza maji ya mabomba katika makazi ya watu, umaskini utatoweka”, Riuki alieleza.

Mama alibakia kimya kwa muda na kumtupia jicho Riuki. Alitambua jinsi alivyokawa na hamasa kuhusiana na suala la maendeleo. Alikumbuka jinsi ambavyo akiwa mwanafunzi, Riuki alipenda kuzungumzia juu ya kusalitiwa kwa ndoto ya uhuru. Aliwalaumu wakuu wa nchi kwa kuyafumbia macho matatizo ya wanancni huku wakijishughulisha kujitajirisha. Ni kama kwamba walitafuta uongozi sio kwa nia ya kuboresha maisha ya wote bali kujinyanyua kitabaka. “Utabiri wa yule mbunge aliyezungumzia uhuru na kunyang’anyana umetimia”, aliwaza. Hatimaye alirudi kwenye mazungumzo na kusema:

“Tutaendelea kukuombea mwanangu. Ufanisi wako ni ufanishi wetu. Wewe sasa ni taa ya kijiji chetu. Utatumulikia njia tutoke kwenye giza la ufukara”.

Riuki alisita kwa muda kama kwamba alikuwa akiwazia jambo fulani, kisha akasema: “Zawadi ulizionaje mama?”

“Zawadi? Zawadi gani” mama aliuliza kwa mshangao.

“Zawadi nilizokuletea”, Riuki alikariri.

Kulikuwa na kimya cha muda.

Juu ya mti mrefu uliokuwa karibu, sauti fulani ilisikika. Matawi yalichezacheza na majani makavu kuanguka. Mara, kupu! Kitu fulani kikaanguka ardhini kwa kishindo.

“Nyoka!” mama alimaka.

Riuki aliokota jiti la kumpondea lakini aliposogea karibu aligundua kwamba ni mfu.

“Labda ni windo la ndege fulani”, alisema, huku akimpinduapindua kwa jiti lake.

“Inawezekana. Kwa kweli niliona mwewe karibu hapa nikielekea mtoni. Mwewe kapata windo, likamponyoka kwa bahati mbaya”, mama alieleza.

Riuki aliinua uso na kuuelekeza angani.

“Mwewe yulee!”alisema huku akiashiria. Sijui kwa nini hashuki kuchukua windo lake?”

“Hawezi kushuka tukiwa hapa. Atakuja tukiondoka”, mama alijibu.

“Tuache mambo ya mwewe na windo lake”, Riuki alisema. “Juzi nimewaletea zawadi, nikamwachia mama akuletee. Nilikuta umetoka kwenda kuokota kuni. Nilichukulia kwamba alishakuletea”, Riuki alieleza.

Wingu la mshangao lilitanda kwenye uso wa mama.

“Labda … labda alisahau”, alisema kwa sauti hafifu. Hakuiamini kauli yake mwenyewe lakini aliitoa kwa kutojua aseme nini. Hakuelewa kwa nini hakupatiwa zawadi yake.

“Kusahau? Utasahau vipi jambo kama hili?” Riuki aliuliza kwa sauti iliyofichua kwamba alikuwa ameudhika. “Nakwenda kumuuliza sasa hivi”, alisema huku akitembea kulekea nyumbani kwa hatua za harakaharaka. Mama alimfuata nyuma kwa mwendo wake wa pole pole. Alipofika, hakuingia kwenye nyumba yake kuutua mkoba wake uliokuwa na makaratasi ya kazini. Alikwenda moja kwa moja hadi jikoni ambamo mamake alikuwa akipika. Alibisha kisha akasukuma mlango na kuingia. Alikaribishwa na wingu la moshi. Alikohoa huku macho yakitoa machozi.

“Samahani mwanangu. Hizi kuni hutoa moshi mbaya”, mamake alisema.

“Unawezaje kukaa ndani kwenye moshi wote huu?”

“Ni mazoea. Upishi na moshi ni marafiki”.

Mama alipuliza moto mpaka ukawaka. Moshi ukapungua na hatimaye kuisha. Alikisukuma kigoda kilichokuwa karibu naye upande wa Riuki ili aketi. Riuki aliketi kisha akaanza mazungumzo.

“Zile zawadi mama ulifanyaje?” aliuliza.

“Sijazipeleka mwanangu. Nimezongwa na shughuli hata sipati nafasi. Nitampelekea. Usiwe na wasiwasi”, mama alijibu.

“Nyumba zenu ziko karibu kama mdomo na pua. Shida ya kutopata nafasi haieleweki. Huhitajiki kufunga safari ya kwenda mbali”.

“Nitampelekea mwenyewe zawadi zake”, mama alikariri.

Riuki alifikiria kuzipeleka mwenyewe lakini alighairi. Ingemfanya mamake afikirie kwamba mwanawe hamwamini.

“Unaendeleaje na kazi?” mama aliuliza ili kubadilisha mada ya mazungumzo.

“Vizuri tu hamna shida. Napatana vizuri na wakubwa na pia wadogo wangu. Nina hamu ya kutumia wadhifa wangu kupigana na umaskini katika eneo hili”.

“Unasema kama wasemavyo watu wa siasa”.

“Wanasiasa husema tu ili kuwalaghai watu kuwapigia kura. Mimi ninayo nia hasa. Wala sitaki kura zozote”, Riuki alisema kwa msisitizo.

“Elimu kubwa unayo; kazi kubwa unayo pia. Ukisema na wakuu wa serikali utasikizwa. Kweli kijiji chetu kimebaki nyuma sana. Hata shule ya msingi hatuna”.

“Tutasukuma mambo. Hatuwezi kukubali kuendelea kuishi namna hii”.

Waliendelea kuzungumza kwa muda. Hatimaye, Riuki aliinuka na kutoka. Alikwenda na kuingia kwenye nyumba yake. Pindi tu alipoingia kwake, alimsikia mamake wa pili akibisha hodi jikoni alikotoka. Aliwaza kwamba labda ameamua kuzifuatilia zawadi zake badala ya kusubiri apelekewe. Mara akasikia majibizano makali kama ya ugomvi. Alishangaa, akatega sikio.

“Umeona mtoto mdogo wa kudanganya hapa? Sema tu ukweli! Unataka kuchukua kila kitu”, mgeni alisema kwa sauti ya juu.

“Nimekwambia nilisahau. Kama hutaki kuamini …”, mwenyeji alijitetea.

“He hee! Hebu sikieni haya jamani! Umekuwa lini bikizee wa kusahausahau kila kitu? Hamna cha kusahau. Uchoyo mtupu! Usituone tumenyamaza ukadhani hatuelewi”, mgeni alipaza sauti.

“Kama mimi ni mchoyo umekuja fuata nini hapa? Si uende kwenye ukarimu?”

“Nakuona tu umenibadilikia siku hizi. Tangu Riuki apate kazi umeanza kujitengatenga nami na kutaka kummiliki. Ukiona nasema naye, unakunja uso. Nini kinakusumbua?” mgeni aliendelea kutoa joto lake.

“Riuki ni mwanangu. Inakuhusu nini ninavyohusiana naye? Unamfuatafuata ukitafuta nini?” mwenyeji alitamka kwa hasira na chuki.

Sasa mgeni alishika kiuno kwa mikono yote miwili kama mchezaji aliyekuwa akijitayarisha kwa ngoma.

“Ooh, sasa amekuwa mwanao eh? Miaka yote hii tukimlea na kumsomesha pamoja alikuwa mtoto wetu. Leo amekuwa mwanao eti kwa sababu ameanza kulipwa mshahara. Unafiki ulioje! Ubinafsi na uovu usio na kifani!” aliteta.

“Mtoto wetu? Kwani tulizaa kikoa? Riuki alitoka humu tumboni mwangu. Asiyekuwa na mwana aeleke jiwe”, mwenyeji alifyatua mishale yenye sumu.

Mgeni aliruka kama aliyeumwa na nge. Alimshika mwenyeji, akamvuta kwa nguvu na kumwangusha. Walibingirishana sakafuni huku wakipigana makofi na kuraruliana nguo. Mapambano yaliendelea kwa muda. Riuki ndiye aliyekuja kuwaamua. Walipotulia kidogo, alimshika mkono mamake wa pili na kumrudisha kwake. Alijutia kumwachia mamake zile zawadi. Angezigawa mwenyewe. Zawadi zilizodhamiriwa kuleta mapenzi na mshikamano sasa zilileta uhasama na farakano.

Tangu siku hiyo, mama zake Riuki walikuwa hawapaliani moto. Riuki aliupuuza uadui wao. Alimnunulia mamake wa pili zawadi kama zile za awali. Akaendelea kumtembelea nyumbani kwake na kuzungumza naye kama zamani. Hata alipohisi kwamba moyo wa mamake wa pili ulishabadilishwa na chuki isiyoelezeka dhidi ya mamake wa kwanza, aliendelea kumpenda. Hakuelewa kwamba mamake wa pili alishapata jeraha moyoni amabalo halingeponyeka. Alikuwa amefumwa vibaya sana na mishale yenye sumu ambayo ilifyatuliwa na kinywa cha mwenyeji wake siku ile ya ugomvi. Siku isiyosahaulika. Mshale ulioleta uchungu mwingi zaidi ni ule wa kukumbushwa kwamba alikuwa tasa. Hili hakuweza kulisamehe.

Jambo ambalo Riuki aliliona kama kichuguu lilikua upesi likawa mlima. Naam. Mlima wa uadui mkubwa sasa uliowatenganisha mama zake. Babake na ami yake walijaribu kuleta suluhu lakini hawakufua dafu. Riuki hakuelewa. Alikataa kuamini kwamba tukio la siku moja liliweza kufuta urafiki wa miaka mingi.

Wakati huu Riuki na mwalimu wake wa zamani, Padre M’Arache walikutana mjini mara kwa mara. Walizungumzia hali mbaya ya kuendelea kupanuka kwa bonde baina ya matajiri na maskini nchini. Ilikuwa wazi kwamba haya yalikuwa matokeo ya uongozi bubu. M’Arache alipenda kuelezea hali ya kisiasa nchini kama “siasa za tumbo”. Watu waliingia katika siasa sio kuhudumu bali kujaza matumbo yao kwa kupora raslimali za umma. Hatimaye Riuki alizua mada ya uadui baina ya mama zake wawili na kumuomba M’Arache ajaribu kuuzima moto wa uadui uliokuwa ukirindima. M’Arache aliahidi kufanya kadiri ya uwezo wake.

Riuki alikuwa mwanakijiji ambaye hakuwa na uanakijiji. Mambo mengi yaliyotokea kijijini aliyapuuza. Hakuwa na wakati wa kuyafuatilia. Wanakijiji walimshangaza kwa mambo mengi. Lakini lililomshangaza zaidi ni tabia ya kujenga uadui mkubwa kutokana na mambo madogo. Ng’ombe alipotoroka kutoka zizini na kuharibu mimea ya jirani, uadui wa kudumu ulijengeka baina ya mwenye ng’ombe na mwenye shamba. Watoto wa majirani walipogombana au kupigana, wazazi wao waligeuka kuwa maadui. Mradi, wanakijiji walitafuta kila sababu kujenga uadui. Yaliyotokea baina ya mama zake wawili yalikuwa matukio ya kawaida, tena ya kila siku kijijini. Riuki aliuona kuwa ujinga mtupu. Alikataa kata kata kuhusishwa na uadui wa kijinga.

Hakuwahi kukaa kijijini na kuingiliana na wanakijiji kwa muda wa kutosha kumwezesha kuwaelewa vyema. Yaani kufahamu saikolojia na mikabala yao juu ya maisha. Sehemu kubwa ya ujana wake, alijishughulisha na masomo yake na uchezaji kandanda. Vijana wa rika lake walipokwenda Ugene kufanya vibarua ili wapate pesa za kununulia sigara, yeye alikwenda kujificha na vitabu vyake. Jioni walipokuwa wakipitapita vichochoroni wakitafuta wasichana, aliwasha taa chumbani mwake na kuvitafuna vitabu kama mtu aliyekuwa na njaa kuu ya elimu. Njaa yake ilikuwa ya kipekee kwa sababu kadiri alivyokula ndivyo ilivyoongezeka. Akamaliza masomo ya shule ya upili. Alikuwa amejiandaa vizuri kwa mtihani wa mwisho kiasi kwamba aliumeza kama uji. Matokeo yalimvika taji la ushindi, njia ya kuingia Makerere ikafunguka. Baada ya kuondoka kwenda Kampala, aliadimika kijijini kama wali wa daku. Wakati wa likizo ndefu alifanya kazi Nairobi au Kampala. Alikuja nyumbani kuwasalimia jamaa kwa siku chache tu.

Alipomaliza masomo na kupata kazi katika makao makuu ya wilaya, aliamua kuishi katika nyumba yake ndogo ya mbao kijijini. Hivyo alilala nyumbani na kurauka kwenda kazini kila asubuhi. Alidhamiria kuendelea kufanya hivi kwa mwaka wa kwanza kazini. Adunduize pesa kisha anunue nyumba yake mjini mwaka wa pili. Kwa ufupi, Riuki hakuwahi kuvuta hewa ya kijijini vya kutosha kuwa mwanakjiji kamili. Mambo kama uchawi, laana na miko chungu nzima yaliyotawala mawazo ya wanakijiji yalikuwa mbali naye kama ardhi na mbingu. Kilichotawala mawazo yake wakati huu ni mipango yake ya kupambana na umaskini. Aliamini kwamba umaskini ndio uliokuwa chanzo cha ujinga, ushirikina uadui, uchochole na ila nyingine nyingi ambazo ziliwakwamisha wanakijiji. Aliona kwamba kuondoa baa la umaskini wa kupindukia kungebadilisha maisha yao.

Riuki alikwa mhubiri wa dini ya elimu na maendeleo. Aliamini kwamba huu ndio mwanga ambao ungeondoa giza la ujinga na umaskini. Lakini dini yake ilikabiliwa na adui mkubwa. Adui huyu alikuwa uchawi. Kweli kijiji cha Gituge hakikuwa na utajiri wa mimea ya kuleta fedha. Kweli kijiji hiki hakikuwa na watu waliotangulia katika shindano kuu la mbio za utajiri baada ya uhuru. Hata hivyo hakingekuwa zizi la umaskini kama si uchawi. Kulikuwa na visa vingi vya wanakijiji wenye bidii kuangamizwa na uchawi. Hivi karibuni, mfugaji maarufu wa kijijini alikufa katika mazingira ya kutatanisha. Usiku alianza kupiga mayowe akisema kuwa maadui zake wanamkaba koo. Mkewe aliwasha taa akajaribu kumwamsha akidhani kuwa mumewe alikuwa katika ulimwengu wa jinamizi. Lakini hakutulia. Aligaragara kitandani huku akitokwa na povu kinywani. Punde si punde alikuwa amekata roho. Huo ukawa mwisho wa Marete aliyekuwa mgawaji mkuu wa mifugo katika vichinjio vya Ugene.

Adui uchawi hakuwasamehe hata vijana wa shuleni. Wachache waliofanya vizuri katika mitihani; waliohitimu katika mafunzo mbalimbali, walihujumiwa na silaha zake. Baadhi yao walishikwa na wazimu, wengine wakaambukizwa magonjwa ya ajabu kama vile kufura tumbo na hatimaye kufa.

Yote haya Riuki aliyasikia kwa mbali kana kwamba yalikuwa yakitokea katika nchi ya mbali badala ya kijijini Gituge. Haikuwahi kumpitikia akilini kwamba yangewea kumfika. Lakini hayawi hayawi huwa. Mke wa baba mkubwa wa Riuki hakupona maradhi ya chuki aliyoambukizwa baada ya ule ugomvi juu ya zawadi. Akaishia kujiunga na jeshi la uchawi. Hii ilikuwa baada ya kuapa kimoyomoyo kwamba mama mwenza hawezi kuendelea kufaidika peke yake kutokana na mali ya mtoto ambaye walimlea pamoja. “Kama ni kupata tupate sote; kama ni kukosa tukose sote”, alijinong’onezea.

Ghafla, Riuki akarukwa na akili. Alizuka kijijini siku moja akiwa uchi. Alikuwa amebeba mafaili ya ofisini.

“Ofisa wa serikali. Serikalikali. Ofisa wa serikali. Atafanyia kazi nyumbani. Sio ofisini tena. Ofisa wa serikali. Atakaa karibu na wananchi. Kijijini,” alibwabwaja.

Watoto walimzomea na kumtupia vijiwe; akina mama wakamkimbia. Tangu siku hiyo hakuingia tena nyumbani. Alishinda juani akizurura njiani na mashambani. Alikesha nje kwenye baridi na mvua. Aliishi hivi kwa miezi mitano. Mwezi wa sita jeshi la uchawi likakamilisha ushindi wake alipokufa. Padre M’Arache – aliyewahi kuwa mwalimu wa Riuki – ndiye aliyeongoza ibada ya mazishi. Sasa alikuwa mzee wa miaka sitini na mitano. Baada ya maiti kufukiwa ardhini, alitoa hotuba ndefu, kali. Aliwakemea wanakijiji kwa “kufuata maongozi ya shetani”. Aliwaambia kwamba kwa kumuua Riuki walikuwa wamezima taa iliyowaongoza kutoka kwenye giza la umaskini hadi kwenye mwanga wa ustawi. “Nyinyi ni watumwa wa uchochole. Mtabaki katika giza la ufukara mpaka mtakapobadilisha mawazo na mienendo yenu”, alimalizia. 

Read more from the May 2013 issue
Like what you read? Help WWB bring you the best new writing from around the world.